Salamu za Rambirambi za Rais Magufuli Kufuatia Kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba, Fidel Castro
Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt, John Pombe Magufuli, amemtumia
salamu za rambirambi Rais wa Jamhuri ya Cuba Mhe. Raul Castro kufuatia
kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba Mhe. Fidel Castro kilichotokea tarehe 25
Novemba, 2016. Katika Salamu hizo Rais Magufuli amesema;
"Nimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Rais Mstaafu wa Jamhuri ya
Cuba Mhe. Fidel Castro. Kwa niaba ya Serikali, Wananchi wa Tanzania na
kwa niaba yangu mwenyewe natoa pole nyingi kwako, familia, Serikali ya
Cuba na wananchi wa Cuba kwa kumpoteza mtu muhimu.
Fidel
Castro alikuwa kiongozi shupavu wa karne, atakumbukwa kwa mchango wake
mkubwa katika ukombozi wa nchi za Kusini mwa Afrika na pia kwa misaada
mikubwa aliyoitoa katika kuboresha huduma za kijamii kwa wananchi.
Alikuwa
rafiki wa Tanzania na Afrika nzima, historia ya Tanzania na Afrika
haziwezi kukamilika bila kumtaja Fidel Castro, hakika kifo chake sio tu
ni pigo kwa Cuba bali pia kwa Tanzania na Afrika.
Naungana
nawe na wananchi wa Cuba katika kipindi hiki kigumu cha majonzi, na pia
nakuombea kwa Mwenyezi Mungu wewe, familia na wananchi wote wa Cuba
muwe na nguvu, subira na ustahimilivu kutokana na kuondokewa na mpendwa
wenu."
Pia Rais Magufuli amemuombea marehemu Fidel Castro apumzishwe mahali pema peponi, Amina.
Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam
Salamu za Rambirambi za Rais Magufuli Kufuatia Kifo cha Rais Mstaafu wa Cuba, Fidel Castro
Reviewed by bloger
on
November 26, 2016
Rating:
No comments