Mkopo elimu ya juu yapeleka kilio UDOM

ZAIDI ya wanafunzi 200 waliodahiliwa katika Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom) kwa mwaka (2016/17), wamelazimika kuacha masomo na kurejea nyumbani baada ya kukosa mikopo ya elimu ya juu kutoka serikalini.
 
Imeelezwa kuwa wanafunzi hao wa mwaka wa kwanza walifika mapema chuoni hapo kabla ya Bodi ya Mikopo ya Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kutoa majina ya wanufaika na wamefikia uamuzi huo baada ya bodi hiyo ’kuwatosa’ kutokana na kukosa sifa za kupata mikopo hiyo.
Aidha, zaidi ya wanafunzi 100 waliokuwa wanaendelea na masomo chuoni hapo wamelazimika kusitisha kwa muda masomo yao kutokana na kuondolewa kwenye orodha ya wanufaika kutokana na kubainika kuwa awali waliingizwa kwenye orodha hiyo pasi na sifa za kupatiwa mikopo.
Saipulani Abubakar, waziri mkuu wa serikali ya wanafunzi chuoni hapo, aliiambia Nipashe jana kuwa kutokana na kukosa mikopo kutoka HESLB, wanafunzi hao wameshindwa kujilipia ada na kumudu gharama za maisha ya chuo na wameamua kurudi nyumbani.
“Nusu ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza wameamua kurudi nyumbani kutokana na kukosa mikopo kutoka serikalini, wengi ni watoto wa maskini, wameshindwa kujilipia na kuamua kurudi nyumbani kufanya shughuli zingine,” alisema Abubakar.
Alisema hadi mwishoni mwa wiki, ni wanafunzi wachache waliosajiliwa chuoni hapo na hawafiki hata nusu ya waliodahiliwa kwa ajili ya mwaka huu wa masomo.
Aidha, Abubakar alisema wapo wanafunzi wanaosubiri hatma yao kutokana na HESLB kupeleka majina kwa mafungu katika vipindi tofauti chuoni hapo. Alisema wanafunzi hao kwa sasa hawakai chuoni na wamekuwa wakiondoka na kurejea chuoni kujua hatima yao.
Alibainisha kuwa miongoni mwa wanafunzi waliorudi nyumbani, wamo waliopata asilimia ndogo ya mikopo ukilinganisha na ada wanazotakiwa kulipa na hawana uwezo wa kumalizia kiasi kilichobaki.
Hata hivyo, kiongozi huyo wa wanafunzi alisema serikali yake iliangalia vigezo vipya vilivyowekwa na bodi na kubaini kuwa baadhi ya wanafunzi wanakidhi, lakini hawamo kwenye orodha ya wanufaika wa mikopo hiyo mwaka huu.
Aliiomba serikali kuangalia upya mustakabali wa wanafunzi hao waliorudi nyumbani kwa kuwa wanapoteza ndoto zao.
“Ni kweli bodi iliweka vigezo vya wanafunzi kupata mikopo, lakini tunashangaa kuona baadhi ya wanafunzi wenye sifa wanakosa, kuna wanafunzi walisoma shule za kata, wengine hawana wazazi na wanaishi vijijini ambako maisha ni magumu na wamenyimwa mikopo,” alisema.
"Wapo baadhi ya wanafunzi waliokosa mikopo hiyo, wakaamua kujilipia ada, lakini kutokana na ugumu wa maisha hasa kukosa fedha kwa ajili ya matumizi ya kawaida, wameamua kuahirisha mwaka ili wakajipange kwa ajili ya mwaka ujao," aliongeza.
NUSU MWAKA
Alisema zaidi ya wanafunzi 100 waliokuwa wakiendelea na masomo lakini waliokosa na kuamua kujilipia ada ya nusu mwaka, walifika ofisini kwake kuandika barua za kuahirisha mwaka hadi pale hali ya maisha itavyokaa vizuri na kuwapa fursa ya kuendelea na masomo.
Alisema kuwa kwa taarifa waliyopewa na HESLB, inaeleza kuwa wanafunzi walioondolewa kwenye orodha ya wanufaika wa mikopo kwa mwaka huu wa masomo licha ya awali kupewa, wamebainika kutumia vyeti feki vya vifo, majina yao kutoonekana kwenye vitivyo wanavyopangwa na kutosaini uthibitisho wa kupatiwa fedha.
Kiongozi huyo pia alibainisha kuwa kuna wanafunzi wanaondelea na masomo lakini hawana uhakika kama wataendelea kunufaika na mikopo hiyo kwa kuwa usajili kwa ajili ya mwaka huu wa masomo umesitishwa kusubiri HESLB itoe majina ya wanafunzi inaoendelea kuwapa mikopo.
Kutokana na hali hiyo, Abubakar alisema serikali ya wanafunzi chuoni hapo imeamua kukutana na Katibu Mkuu Wizara ya Elimu, Sayansi, Teknolojia na Ufundi, Maimuna Tarish na Mkurugenzi wa HESLB, Abdul- Razaq Badru, Novemba 20, mwaka huu kuzungumzia hatima ya wanafunzi waliokosa mikopo.
Alipotafutwa na gazeti hili jana, Mkurugenzi Msaidizi wa Habari, Elimu na Mawasiliano wa HESLB, Cosmas Mwaisobwa, alisema wanafunzi watakaopata fedha mwaka huu ni wale waliokidhi vigezo vilivyowekwa.
Alisema bodi imefanya uchambuzi yakinifu wa kujua nani anastahili kupata mikopo hiyo na nani hastahili.
Mwaisobwa alisema bodi haiwezi kutoa msaada wowote kwa wanafunzi waliokosa mikopo na kuamua kurejea nyumbani kwa kuwa kutokana na mfumo wa kielektroniki uliotumika kufanya uchambuzi, imeweza kubaini wanafunzi wenye sifa na wasio na sifa.
Mwaisobwa alisema “Sisi tunafuata sifa na vigezo vilivyowekwa vya utoaji wa mikopo, hata kama wangerudi wote nyumbani, tunachoangalia ni vigezo vya kupata huo mkopo”.
Alisema mwaka wa masomo 2016/17 Udom ulianza Oktoba 29, mwaka huu na kwamba baadhi ya wanafunzi wa mwaka wa kwanza waliobahatika kupata mikopo, walipewa fedha kwa ajili ya chakula na malazi Ijumaa iliyopita.
Hivi karibuni, HESLB ilitangaza kuwaondoa zaidi ya wanafunzi 3,000 kwenye orodha ya waliotarajiwa kunufaika na mikopo hiyo kwa mwaka huu wa masomo kutokana na kile ilichokielezwa kuwa ni kupungukiwa sifa.
Mkurugenzi Mtendaji wa HESLB, Abdul-Razaq Badru, alisema mbali na kuondoa wanafunzi hao, wengine 87 ambao awali hawakujumuishwa kwenye orodha ya wanufaika kutokana na sababu mbalimbali ikiwamo kusoma shule zisizo za serikali, sasa watapata mikopo baada ya kubainika walisomeshwa na wafadhili.
Taarifa iliyotolewa na Badru Oktoba 30, ilibainisha sifa za wanufaika wa mkopo kuwa ni wanafunzi yatima na walemavu, wanaotoka familia za hali duni hususani waliosoma shule za umma na wale wanaosoma fani zilizo kwenye kipaumbele cha taifa.
Fani hizo ni sayansi za tiba na afya, ualimu wa sayansi na hisabati, uhandisi wa viwanda, kilimo, mifugo, mafuta na gesi asilia.
Fani nyingine ni sayansi asili huku ya mwisho ikiwa ni sayansi ya ardhi, usanifu majengo na miundombinu.
Katika mwaka huu wa masomo, upangaji wa mikopo hiyo unazingatia bajeti ya Sh. bilioni 483 zilizopitishwa na Bunge zikitarajiwa kunufaisha wanafunzi 119,012, kati yao 25,717 wakiwa ni wa mwaka wa kwanza na 93,295 wanaoendelea na masomo yao.
Mkopo elimu ya juu yapeleka kilio UDOM Mkopo elimu ya juu yapeleka kilio UDOM Reviewed by bloger on November 14, 2016 Rating: 5

No comments

Business

Post Navigation Display